Mourinho ajutia kukosa makali kwa Chelsea
Mourinho ajutia kukosa makali kwa Chelsea

Posted in News on Feb 12, 2014.

Meneja wa Chelsea Jose Mourinho aliachwa akijutia kushindwa kwa timu yake kuua mechi baada yao kulazimishiwa sare ya 1-1 wakiwa West Bromwich Albion mnamo Jumanne na wakapoteza fursa ya kufungua mwanya wa alama nne kileleni mwa Ligi ya Premia.



Chelsea, waliokuwa wameshinda mechi tisa kati ya 11 walizocheza karibuni katika mashindano yote, walitarajia kushinda timu hiyo ya West Brom ambayo ni miongoni mwa timu tatu zinazoshika mkia ligini.



Viongozi hao wa ligi walionekana kudhibiti mambo hadi muda mfupi kabla ya mechi kuisha na kutoweza kwao kukabiliana na presha kulisikitisha Mourinho.



"Dakika 20 za mwisho walituwekea presha na wakafunga bao. Labda walistahiki alama hiyo moja. Alama ni alama na mwisho wa msimu tutaona,” aliambia BBC baada ya timu yake kufikisha alama 57.



“Ninafikiri mechi hiyo kwa dakika 60 ilikwua mikononi mwetu, West Brom hawakukanyaga eneo letu la hatari. Hatukuweza kuua mechi.”



Mreno huyo wa miaka 51 amekuwa akipuuzilia mbali uwezekano wa Chelsea kushinda ligi akiwataja kuwa ‘farasi mdogo’ katika kinyang’anyiro chenye Arsenal walio nambari mbili, alama mbili nyuma, na Manchester City, walio alama nyingine nyuma katika nambari tatu.



"Nilikuwa nahisi kwamba jambo pekee ambalo tungeweza ni kujilinda vyema. Hatukuwa na nguvu za kutosha kuvumilia dakika 10 za mwisho. Mechi huwa haijaisha hadi kipenga cha mwisho na kosa katika kujilinda lilisababisha bao hilo,” akaongeza.



TORRES AREJEA



Mourinho angalau alikuwa na kitulizo kumkaribisha tena straika Fernando Torres, aliyeingia kama nguvu mpya dakika ya 69 kuchukua nafasi ya Samuel Eto'o, baada yake kukaa nje kutokana na jeraha la goti tangu Januari 19.



“Ni mchezaji mmoja mbadala. Mwezi uliopita tumekuwa tu na Eto'o na Demba (Ba)," aliambia Sky Sports. "Tukiwa nao wote basi tutakuwa na zaidi ya tunaohitaji.”



Kocha wa West Brom Pepe Mel alsiema timu yake ingetwaa alama zote tatu lakini ilihitaji kusawazisha mapema.



“Nimefurahi sana. Wachezaji walitia bidii na walikuwa na nguvu. Kama tungefunga la kwanza mapema tungeshinda mechi hiyo,” alisema.



"Chelsea walikuwa mbele, kwangu leo imekuwa siku njema. Wachezaji walicheza vyema sana na, kwa hakika, kama tungefunga kabla yao, tungeshinda mechi hii.”



Tangu Mel achukue usukani kutoka kwa Steve Clarke Januari, West Brom wamepokonya alama Everton, Liverpool na sasa Chelsea licha ya kuwa nyuma na anaamini kwamba watanusurika mwisho wa msimu.



“Moja-moja dhidi ya Everton, Liverpool na Chelsea. Sasa tunahitaji kushinda mechi ijayo. West Brom itakuwa kwenye Ligi ya Premia,” akasema.

Share this article: